Siasa
 

NJIA YA KWENYE KIFO YENYE MAVUMBI

Asubuhi ya Jumapili ya Juma lililopita, Mahmoud Shawara, kibarua, alipanda nyumbu wake na akatoka nyumbani kwake katika kijiji cha Nuaman kwenda kutafuta kazi katika kijiji cha jirani cha Umm Touba. Majira ya kama saa 3.00 asubuhi alikamatwa na Polisi wa kituo cha Mpakani ambacho kinawaweka kizuizini wafanyakazi ambao hawana kibali cha kuingia Israel kila asubuhi.

Askari hao wa mpakani walimuamuru Shawara kuingia kwenye gari lao aina ya Jeep. Yeye akakataa. Hakutaka kumuacha nyumbu wake bila uangalizi. Majira ya saa 3:30 asubuhi kaka yake alimuona kwa mara ya mwisho akiwa mwenye afya na timamu. Mnamo saa 10 jioni, mkazi wa Umm Touba aitwaye Mohammed Hamadani alimuona nyumbu akienda shoti kuelekea hapo kijijini na akiwa anaburuza kitu fulani nyuma yake. Kutoka mbali kidogo Mohammed Hamadani alifikiria ingeweza kuwa chuma kilichochakaa. Jinsi farasi yule alivyozidi kusogea karibu, Mohammed Hamadani aliweza kuona kwamba alikuwa anaburuza mtu aliyejeruhiwa kapondwa-pondwa. Nyumbu yule, yeye anasema, alikuwa anakwenda shoti kushuka kilima na alionekana aliyetishwa. Alimsimamisha mnyama huyo na kisha akagundua kwamba yule mtu aliyekuwa akiburuzwa kwenye ardhi alikuwa ni Mahmoud Shawara, kutoka kijiji cha jirani ambaye alikuwa anamtambua vizuri. Mkono wa kushoto wa Shawara ulikuwa umefungwa kwenye shingo ya nyumbu huyo. Alikuwa hanafahamu na akipumua kwa shida. Fuvu lake na uso vilikuwa vimepondeka upande wa kushoto na alikuwa akitoka damu. Aliweza kutamka maneno machache yaliyokatika katika, yasiyoeleweka vizuri au sehemu za maneno kisha akafunga pumzi.

Hamadani alimfungua kamba Shawara, akamlaza chini na akamminya kifuani mwake ili kumrudishia pumzi yake. Kisha akaita gari la wagonjwa kutoka kwenye kliniki ya kituo cha afya cha shirika la matengenezo la Mauhedet kijijini hapo. Shawara alipelekwa kwenye kituo cha afya huko Ein Kerem, Jerusalem ambako alilazwa katika sehemu ya tiba ya Nyurolojia ya kitengo cha wagonjwa mahututi. Mwishon mwa wiki, ambamo hakupata kurudiwa na fahamu, Shawara alifariki kutokana na majeraha yake. Alikuwa na umri wa miaka 43, mfanyakazi na baba wa watoto tisa, aliyekuwa amekwenda kutafuta kazi katika kijiji cha jirani.

Shawara aliuawa vipi? Je, Polisi wa mpakani walimtesa kimwili na kumfunga kwenye mnyama kisha wakamtishia mnyama huyo akimbie na kusababisha kifo chake kutokana na mapigo kwenye kichwa kwenye mawe vile mnyama huyo alivyokuwa akienda mrama kushuka kilima hicho? Je, alipigwa kisha kafungwa kwenye nyumbu huyo, ambaye baadae aliswagwa kuchukua njia yake? Au Idara ya upelelezi ya Polisi wa Wizara ya Sheria wako sahihi katika kudai kwamba hii ilikuwa ni ajali ya upandaji wa nyumbu – Shawara alijifunga mwenyewe kwenye nyumbu, akaanguka toka juu yake na akaumia vibaya sana.

~Juu

Watu hapo Nuaman walituambia juma hili kwamba Polisi hao wa mpakani kwa kawaida huwafunga kamba watu ambao wamo ndani ya Israeli kinyume cha sheria (shabahim) kwenye wanyama wao. Tutataja ushahidi wa mfanyakazi mwingine Mpalestina ambaye alifungwa kwenye punda wake na Polisi wa mpakani majuma machache yaliyopita kama alivyokuwa amelala chini aridhini, uso ukiangalia chini na mikono yake ikiwa imefungwa nyuma ya mgongo wake na pande la mkaa mgongoni mwake likiwa limewekwa hapo na Polisi wa mpakani. Katikati ya Nuaman na Umm Touba, vijiji viwili vyenye amani juu ya bonde la kustajabisha, ndipo lilipo eneo hilo la kuburuzia.

Picha ya karibu ya tishio hilo: Uso wa yule mtu aliyeuawa umepondwa. Mwili wa Shawara umelala sakafuni nyumbani kwake, ukiwa umefunikwa na bendera ya Palestina na shuka kutoka kituo cha afya cha Shaare Zadek, Jerusalemu (ingawaje alifia Hadassah). Nyumba hiyo – jengo lisilo halali – haina paa, isijekuwa ingebomolewa na Israeli. Turubai la rangi ya buluu limefunika makazi hayo kuyalinda dhidi ya hali ya hewa.

Ni wakati wa mchana, dakika chache kabla ya shughuli za mazishi zianze, siku ya Jumapili ya Juma hili. Mtu mmoja anaweka bendera ya Hamas kwenye mwili wa marehemu,juu ya ile bendera ya Palestina na lile shuka la Shaare Zedek. Wanawake wa familia hiyo wanalia visivyotulizika; yule binti mkubwa, Kauther, 24, yuko karibu kuzimia. Kabla mwili kutolewa chumbani, ule uso, ukiwa umefunikwa isivyo kawaida, ili kuficha yale majeraha. Gavana wa Bethelehem, Salah Taamri, amesimama hapo nje pamoja na watu maarufu wa hapo. Mazishi yamezuiwa, magumu. Kuna ukelele mmoja tu wa siasa kali Ewe Yahudi, Ewe Nguruwe, tutakukanyaga chini ya miguu.

Wanakijiji hao wameshawishika kwamba Shawara alikuwa ameuawa na Polisi wa mpakani. Lakini pale jeep la Polisi wa mpakani inapojitokeza ghafla katikati ya mazishi, kwa mtazamo wa juujuu wa uchokozi, kule kuzuiwa kunadumishwa. Hii ndio tabia ya hawa watu wa kilimani: Wanashindwa kuongea na wenye wasiwasi sana. Nuaman iko kwenye barabara ya wazi ya kwenda Jerusalem, katikati ya Bethelehem na mji mkuu wa Israel, mashariki ya ujirani wa Har Homa katika sehemu ambayo ule ukuta unaotenganisha bado haujakamilika. Polisi wa mpakani wapo hapa kila siku na watu wanaogopa kuongea.

Wiki moja kamili kabla, Shawara aliondoka nyumbani kwake kwa mara ya mwisho. Ndugu yake, Daoud, aliondoka nyumbani kwake karibu ya saa 1:30 kwa miguu, akielekea Umm Touba, ambayo ipo ndani ya mipaka ya manispaa ya Jerusalem, na ambapo wakati mwingine kazi hupatikana katika ujenzi au Shambani. Daoud anasimulia kwamba baada ya muda mfupi, jeep ya Polisi wa mpakani ilitokea na kumkamata yeye na wale vibarua wengine, jumla yao wakiwa sita, ambao walikuwa wametoka hapo kijijini. Hakuna hata mmoja wao aliyekuwa na kibali cha kufanya kazi Israel. Sio muda mrefu baadaye, Mahmoud akawasili pia, akiwa amepanda nyumbu. Yeye pia alikuwa njiani kwenda kutafuta kazi kama ilivyokuwa desturi yake ya kila siku.

Wale Polisi wa mpakani walimuweka kizuizini pia. Walinyang’anya kile kitambulisho cha manjano cha kila mtu katika kikundi hicho na wakawaamuru kwenda kituo cha Polisi cha Talpiot, katika sehemu ya kusini ya Jerusalem. Baada ya majadiliano kiasi, Daoud anasema, wale Polisi wa mpakani waliwapeleka huko kituoni kwa jeep yao. Mahmoud alikataa kuingia kwenye jeep hiyo, akisema kwamba asingeweza kumuacha yule nyumbu peke yake pale peupe. Mabishano yakatokea, lakini wale Polisi wa mpaka hawakutumia nguvu dhidi ya Mahmoud, anasema ndugu yake Daoud. Daoud alichukuliwa kwenye jeep na ndugu yake akabakia pale na yule nyumbu na wale Polisi wa mpaka waliobakia naye. Baada ya mahojiano mafupi na baada ya kuweka saini ahadi ya kutoingia tena Umm Touba, Daoud na wale wengine walipelekwa kwenye kituo cha ukaguzi kipya cha Rachel – kule kwenye kaburi la Rachel, karibu na lango la kuingilia Bethelehem – na wakatupwa kwenye njia yao.

~Juu


Daoud hakumuona ndugu yake tena akiwa hai. Akirudi kijijini karibuni saa 6:30 mchana, hakuweza kumuona Mahmoud. Ni kijiji kidogo cha watu 170, msiba mmoja hadi juma lililopita, nyumba za mawe ukingoni mwa bonde la kustaajabisha upande wa mashariki, makazi ya Har Homa upande wa magharibi. Ni mabedui, watu wa kabila la Taamra.

Saa 10 jioni Mohammed Hamadan alimuona yule nyumbu anayekwenda shoti, akiacha vumbi nyuma yake. Alikuwa anapita katika ile njia ambayo inashuka kuelekea Umm Touba ambayo imezungukwa pembeni na marundo ya takataka. Sasa tunatembea katika ile njia kutoka Nuaman kwenda Umm Touba, njia ambayo yule nyumbu aliifuata angalau kwa sehemu yake tu. Ni njia yenye mawe mawe. Mita mia chache tu zinateganisha ile sehemu ambayo Shawara alikamatwa na ile sehemu ambayo aligunduliwa akiwa amefungwa kwenye nyumbu. Saa sita na nusu zinatenganisha ule muda ambao kwamba ndugu yake Shawara alimuona akiwa hai na mzima na ule muda aliogunduliwa akiwa amefungwa kwenye nyumbu. Hakuna anayejua ni nini kilichotokea katika masaa yale.

Hamadan sasa anatafuta dalili za damu katika ile njia iliyofuatwa na yule nyumbu, lakini mvua kwa dhahiri ilikuwa imefuta kila kitu. Hakuona majeraha katika mwili wa Mahmoud, ni katika ule upande wa kushoto wa kichwa chake uliopondwa tu. Alikuwa amefungwa kwenye nyumbu kwa kamba ya nguo nyeusi. Hapa ndipo pale alipomsimamisha yule Nyumbu, akizikamata hatamu zake kwenye ule mteremko. Wafanyakazi katika lile ghala la jirani la vifaa vya ujenzi pia waliliona tukio hili. Mwenye shughuli ile alikuwa ni Ahmed Abu Their, ndiye aliyeita gari la wagonjwa. Yeye anasema kwamba alimuona Mahmoud akiwa amefungwa kwenye Nyumbu lakini aliogopa kusogelea.

Wanaume nyuso zao zikiwa na hofu, wamekaa katika mgongo wa sehemu iliyoinuka na wanaisubiri ile gari ya wagonjwa ilete ule mwili kutoka Hadassar. Wanawake, katika mavazi meusi wamekaa katika kivuli cha nyumba ya yule mtu aliyekufa na wanaomboleza. Vijana wanapeperusha bendera za Palestina katika mapaa ya nyumba na katika wigo wa eneo la makaburi ambalo liko chini ya kijiji hicho.

Msafara unakaribia kutoka kwenye bonde, lile gari la wagonjwa la Wapalestina likiwa mbele na taa nyekundu zimeweka mweka. Jeep ya kijeshi ya Israeli inaangalia kwa mbali, ikiwa imesimama kwenye barabara ya usalama iliyotiwa kibamba sambamba na ule ukuta unaotenganisha ambao unajengwa kama kinga ya Jerusalem. Hakuna hata mmoja hapo kijijini anayejua ulipo mpaka kati ya maeneo hayo na Jerusalem. Hapo ukuta huo utakapokamilika yote yatakuwa wazi. Hapo Nuaman ni mkazi mmoja tu aliye na kitambulisho cha kadi ya buluu cha Jerusalem, kila mtu mwingineo ni kitambulisho cha “Maeneo.” Jirani ya Umm Touba ni Jerusalem lakini sio wakazi wote wenye kadi za buluu. Mtu mmoja karibu yangu anafuta chozi. Mwili unatolewa kwenye gari la wagonjwa kuingizwa ndani ya nyumba. Huko ndani uso wa marehemu unafunuliwa, uso wa mkulima mdogo, ulio na sharubu ndefu, uliojeruhiwa – na mara unafunikwa haraka.

Mwanasheria wa kijiji, Daoud Darawi, anayefanyakazi katika tawi la Palestina la Ulinzi kwa watoto kimataifa (DCI) Ramallah, anadai uchunguzi wa kimataifa juu ya mazingira ya kifo cha Shawara. “Walimfanyia yeye kile wazungu walichowafanyia wahindi huko marekani,” anasema. Anaelezea juu ya masuala mawili kama hayo. Katika kijiji cha karibu cha Dar Salah, Polisi wa mpakani wakiwa ndani ya jeep walimshambulia punda ambaye juu yake alikuwa amepanda Walid Amiya, wakimuangusha chini. Alinusurika. Katika kijiji cha karibu cha Wadi al-Humos walimfunga Maamoun Abu Ali kwenye punda wake na wakajaribu kumfukuzia kwenye njia yake mnyama huyo. Yeye pia alinusurika. (Tutamrudia baadaye).

Kwa mujibu wa wakili Darawi, hao Polisi wa mpakani wamekuwa hapo kwa takriban mwezi mmoja. Tangu kuwasili kwao, matukio ya kuwatesa vibarua wanaotafuta kazi katika kijiji cha jirani yamezidi. ‘Njoo siku moja majira ya saa 11 asubuhi na utaona ni nini kinachotokea hapa kila siku na hawa Polisi wa mpakani,’ mwanasheria huyo anasema. Familia ya Mahmoud Shawara iliandikisha malalamiko kwenye Idara ya upelelezi ya Polisi (PID).

Msemaji wa Wizara ya Sheria, Yaacor Galant, alisema wiki iliyopita kwa niaba ya PID: ‘Uchunguzi wetu mzuri sana, ambao tumeufanya kuanzia pale malalamiko haya yalipopokelewa mpaka Ijumaa iliyopita, wakati wa mchana, unaonyesha kwamba hakuna uhusiano kati ya shughuli za Polisi wa mpakani na kuumia na kufa kwa mtu huyu. Ni dhahiri kwamba alionywa kuhusu nyumbu huyo, akaambiwa asimpande. Alikuwa ni nyumbu wa porini. Ni dhahiri kwamba alimpanda, akamuendesha na pia akajifunga mwenyewe kwenye nyumbu huyo.’ Je, uchunguzi umekamilishwa sawasawa? Gallant aliahidi kufuatilia na kurejea kwangu muda mfupi baadaye. Kwa wakati huu hakuna lolote jipya.

Hatujapata ushahidi utakaohusisha polisi wa mpakani (na tukio hili). Tutafurahi kupokea ushahidi mwingine. Kwa wakati huu hakuna anayeweza kuelekeza kwenye uhusiano makhsusi baina ya Polisi wa mpakani na suala hili.

Maamoun Abu Ali ni mfanyakazi wa ujenzi katika jengo ambalo linapanda katika ujirani wa Doha katika sehemu ya kusini ya Bathelehemu. Tulimfuata Jumanne ya wiki hii. Kapera mcheshi wa miaka 20, alikuwa bado anayo makovu ya mapambano yake na Polisi wa mpakani katika lile bonde chini ya Nuaman. Abu Ali anatoka kwenye kijiji cha jirani cha Abadiya. Kama miezi miwili iliyopita, wakati wa Ramadhani, alikuwa amempanda punda wake akiwa njiani kuelekea kijiji cha karibu cha Wadi Humos kununua kuku kwa ajili ya kifungua kinywa kwenye duka la nyama la Shahar. Ilikuwa ni muda kidogo baada kuingia adhuhuri. Mara jeep ya polisi wa mpakani ikasimama karibu yake. “Unakwenda wapi?” Abu Ali aliulizwa, na yeye akajibu; “Nakwenda kununua kuku.” Polisi wa mpakani akakagua vile vitu ambavyo punda alikuwa amebeba halafu akachunguza makaratasi ya Abu Ali, Shabah, na Bingo.

~Juu


Kwa zile hatamu za mnyama huyo wakamfunga mikono Abu Ali nyuma ya mgongo wake na wakamfanya alalie tumbo lake juu ya ardhi, uso chini. Polisi wa mpakani wanapenda kuwaadhibu shabahim wanaowakamata. Abu Ali anasimulia kwamba walimfunga kipande cha gogo la mkaa mgongoni mwake kisha wakamchapa yule mnyama kumfanya atembee. Punda wa Abu Ali ni mzee na ni mbishi, au labda anamtii bwana wake tu – vyovyote iwavyo, alikataa kusogea. Abu Ali anasema yeye pia alivuta kwa mikono yake iliyofungwa ili punda huyo asisogee. Sio vigumu kukisia ni ini kingetokea kama punda huyo angebabaika na kuanza kwenda shoti, na Abu Ali alikuwa amelala uso chini, mikono imefungwa mgongoni kwake mnyama huyo. Wakati mmoja Polisi wa mpakani pia alisimama mgongoni mwa Abu Ali, mguu mmoja juu yake na mwingine kwenye kigogo cha mkaa, ili kumbana.

Unyanyasaji uliendelea kwa takriban robo saa, Abu Ali anasema. Hatimaye wale Polisi wa Israeli walikata tamaa kumfanya yule punda mbishi asogee na wakamuamuru Abu Ali kusimama. Waliongea Kiarabu. Abu Ali anasema kwamba mmoja wao alimfunika macho yake kwa mikono yake na yule mwingine akampiga mara moja usoni mwake kwa jiwe. Bado ana kovu upande wa kulia, chini ya mdomo wake. Walimtishia wakimwambia kwamba kama angezurura hapo tena atauawa. Kisha wakamuelekeza kwenye njia yake. Abu Ali hakusajili mashtaka kwenye Idara ya upelelezi ya Polisi. Alitaka alalamike kwa Polisi wa Palestina halafu wao wayafikishe malalamiko hayo lakini alishauriwa kutokufanya hivyo na Polisi mmoja wa kijiji chake, ambaye alimwambia: ‘Watu wanauawa hapa, hivyo shukuru kwamba uko hai na mwenye afya.’

Wacha tuuambie ulimwengu kwamba kile wanachotufanyia sisi, kuhusu yale maisha ya karaha ya kumilikiwa kiharamu, Mzee Mohammed Abu Ranar Adum, mmoja wa wakuu wa kijiji hiki anasema katika maneno yake ya kusifia. Mazishi yanakaribia kutawanyika kimya kimya. Katika kivuli cha mizeituni, ukingoni mwa kijiji hiki, kando ya bonde, amesimama nyumbu, aliyefungwa kwenye mti. Mnyama wa rangi ya hudhurungi mwenye nguvu. Tunaposogelea kuchukua picha yake, nyumbu huyo anaonyesha dalili ya kutaharuki, anageuza kichwa chake upande na anajaribu bila mafanikio kujifungulia kuwa huru.

Mwandishi wa makala hii ni
Gideon Levy wa Haarez

   
   Vitabu vya Kiarabu
» Orodha ya bei ya Vitabu vya Kiarabu
 
 
  Copyright © Alitrah, 2003. All rights reserved